Katika gazeti Daily News, la Mei 23, 2012 ukurasa wa pili kuna habari kuwa “sheria kuhusu vifo vya akina mama wajawazito” (Law on maternal mortality in the offing”) itakayojulikana kama “Bill to Enact Safe Motherhood Law 2012” iko mbioni kutungwa. Katika habari hiyo Meneja wa Mradi wa shirika la Marekani “Care International”, Bwana David Lyamuya katika mkutano wake na baadhi ya viongozi wa dini alisema kuwa Tanzania inahitaji sheria zitakazomwaadibisha yeyote yule akayebainika kuwa amehusika na kifo cha mwanamke au mtoto mchanga kutokana na uzembe kama hatua ya kudhibiti vifo vitokanavyo na uja uzito na watoto wachanga.
Anasema kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuwa na sera nyingi zenye kulenga kuwalinda wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki ya kupata huduma za kuokoa maisha yao, lakini kwa vile sera hizo sio sheria, watu wamezivunja bila kuadhibiwa. Bwana Lyamuya amewaeleza baadhi ya viongozi hao wa dini kuwa sheria inamruhusu aliyekosewa kuchukua hatua za kisheria, wakati sera haina nguvu ya kumchukulia mkosaji hatua za kisheria.
Pamoja na jitihada za Serikali kutoa huduma nzuri za uzazi katika hospitali, vituo ya afya na zahanati zilizotapakaa nchi nzima hata vijijini, na tukumbuke pia kuna hospitali, vituo vya afya na zahanati zinazomlikiwa na taasisi za kidini na watu binafsi ambazo nazo zimetapakaa nchi nzima, Bwana Lyamuya anadai kuwa ni asilimia 50 tu ya wanawake wajawazito huhudumiwa na wahudumu wa afya waliosomea. Kwa maneno mengine asilimia 50 ya wanawake wajawazito hujifungua bila wahudumu wa afya.
Naye Mratibu wa “White Ribbon Alliance on Safe Motherhood”, Rose Mlay alitoa changamoto kwa viongozi hao wa dini kuunga mkono mswada huo kwa vile umelenga kutekeleza huduma za kijamii ambazo ni muhimu katika dini zote. Akiongea katika mkutano huo Mratibu wa Programu wa “Care International”, Aba Williams aligusia viwango vya juu vya vifo vya wanawake wajawazito kinyume na Malengo ya Milenia.
Inasemekana kuwa sheria hiyo inatokana na mapungufu katika sheria zilizopo; kwa mfano, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu ndoa za wasichana wa umri mdogo; Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ambayo haitoi kinga kwa wanafunzi wasichana wanaopata ujauzito; Sheria ya Watoto ya mwaka 2009 ambayo haina nguvu ya utekelezaji; Sheria ya Wafungwa ya mwaka 1967 ambayo haiongelei masuala ya Afya ya Kizazi kwa wafungwa wanawake; vilevile Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 ambayo haiweki mkazo katika haki za kiafya, kama vile haki ya kupata matibabu kutoka kwa mhudumu mahiri.
Kama yote yatatendeka kama ilivyopangwa, Mratibu wa Kiufundi katika masula ya Utawala na Uenezi, Rachael Boma, anasema kuwa mswada huu utapelekwa Bungeni kwa kusomwa kwa mara ya kwanza mwezi Septemba mwaka huu ikiwa ni hatua ya awali kupelekea kutungwa sheria hiyo.
Taarifa hiyo katika gazeti la Daily News ina mapungufu mengi. Kwa mfano hatujaambiwa idadi ya viongozi wa dini walioshiriki na walitoka katika dini na madhehebu gani, walikuwa na vyeo gani; maaskofu, mapadre, wachungaji, mashehe, maimamu, wainjilisti; kwa uwiano gani. Kwa mfano, mwandishi angetueleza walikuwa viongozi wangapi Wakatoliki, Waangalikana, Walutheri, Wamorovian, Wasabato, Wa-Assemblies of God, Wapentekoste, Wahamadiya, Wasuni, Wahindu, n.k,. Nayahoji haya kwa sababu za msingi, katika kualika watu ili wakubaliane na mambo maovu, yawezekana wakakodiwa watu wowote wale, wakalipwa fedha nyingi, wakaelezwa unayotaka kuyaeleza, wakaupigia makofi na wakaondoka. Nawe waweza kujigamba kuwa umefanikiwa. Katika habari ile hatujasikia maoni ya viongozi hao wa dini, je walikubaliana na walichoambiwa au kama walikuwa na maoni yao tofauti na ilivyoandikwa. Na kwa vyovyote vile, kwa jinsi taarifa ilivyotolewa inaonekana viongozi hao wa dini walipinga hicho walichoambiwa na mwandishi aliona sio vema kuandika maoni yao katika gazeti.
Kabla ya kusema jinsi viongozi wa dini walivyodanganywa, napenda nisema kuwa takwimu huweza kutengenezwa kwa ajili ya kuthibitisha nadharia au mawazo fulani. Mtu mwovu anatengeneza takwimu ili kufanikisha jambo fulani ovu. Kwa mfano takwimu kuwa wanawake wanaopata huduma za kujifungulia mahali bora na wahumu bora wa afya ni asilimia 50 tu, ni za kuzitilia mashaka. Na kama hilo ni kweli, basi tunaaminishwa kuwa jitihada za serikali, taasisi za kidini na watu binafsi katika kutoa huduma za uzazi salama kupitia hospitalini, zahanati au kliniki zilizotapakaa nchi nzima ni za bure. Na baada ya kutupatia takwimu zenye kutia shaka katika jambo hilo, zinafuata takwimu nyingine zenye kutiliwa mashaka; wanawake wanaofariki kutokana uzazi usio salama eti ni 454 kwa 100,000. Takwimu hizi zimetengenezwa kwa makusudi ili zitumike kuthibitisha mambo ambayo viongozi wa dini hawakuelezwa katika mkutano ule.
Ninadhani viongozi wa kidini walioalikwa hawakuelezwa yafutayo:
Katika sehemu ya I inayohusu maelezo ya awali:
“emergency contraception” ; yenye kumaanisha kuwa vidhibiti mimba vinavyotumiwa na wanawake kufuatia tendo la ngono lisilokuwa na kinga ambayo huzuia mimba isiyotarajiwa. Hiyo ina maana kuwa mimba inatungwa, lakini kwa vile haikutarajiwa, basi inazuiwa kuendelea kukua. Maana yake ni kuwa vidhibiti mimba hivyo huzuia mimba kujipandikiza, na hivyo mimba hiyo inakosa hewa na chakula na inakufa; inatoka nje pamoja na damu ya mwezi
“harmful practices”; ikimaanisha desturi mbovu za kidini au kimila zinazoathiri afya ya ujinsia na afya ya kizazi ya wanawake na wasichana. Nina hakika kama hili lingesemwa, viongozi wa dini wangependa kujua vitendo hivyo viovu ni vipi.
“termination of pregnancy”; yenye kumaanisha kukatakata na kutoa nje kwa njia za kikemikali au upasuaji, masalia yaliyomo tumboni mwa mwanamke mja mzito kabla ya kuanza uchungu wa kuzaa. Hapa nina hakika viongozi wa dini wasingekubali kwani vitendo vya kutoa mimba vinapingana moja kwa moja na mafundisho ya dini kuhusu uhai wa binadamu na jukumu la kila binadamu kuulinda uhai wa watoto kabla ya kuzaliwa
Katika sehemu ya II inayohusu upatikanaji wa vidhibiti mimba na uzazi wa mpango:
Nitawashangaa viongozi wa dini watakaokubaliana na dhana kwamba serikali ihakikishe uhuru wa kila mtu kudhibiti kizazi chake. Serikali inahitaji watu ili kujenga uhalali wa kuwako kwake. Kama serikali inaamua kuweka programu za kudhibiti kizazi cha watu wake ina maana kuwa serikali ya aina hiyo imejichagulia njia ya kujiangamiza yenyewe na kuangamiza nguvu za kiuchumi, kijeshi na hata kuangusha mifumo ya kijamii. Viongozi wa dini hawawezi kushiriki mipango itakayowapunguzia idadi ya waamini na hata kusababisha kufungwa nyumba za ibada kama inavyotokea katika nchi za magharibi hizi sasa. Nchi hizo zilikumbatia sera za kudhibiti kizazi cha watu wao kwa miaka mingi ya nyuma.
Viongozi wa dini wangepinga kumweka Waziri wa Afya awe mwamuzi katika masuala ya uzazi katika familia; wangesema kuwa masuala ya uzazi yako katika mamlaka ya watu wa ndoa. Serikali haina mamlaka ya kuingilia masuala ya kudhibiti kizazi kwa wanandoa. Kwa nini viongozi wa dini wafurahie ubeberu wa kimagharibi unataka kutawala hata masuala nyeti ya kizazi cha wanandoa? Huko ni kukiuka haki ya faragha ya wanandoa juu ya maisha yao.
Nadhani pia viongozi wa dini wangepinga wasichana wadogo [adolescent girls] kupatiwa huduma za uzazi wa mpango kwani hao bado wako shuleni. Jukumu la wasichana hao wakati huu ni wa kusoma, kupata elimu ili kuwaandaa kwa maisha ya baadaye. Ukiwachanganya watoto hawa katika masuala ya ngono kwa kutumia vidhibiti mimba uwezo wao kwa masomo unaharibika na mimba za utotoni zinaongezeka kutokana na baadhi yao kushindwa kutumia au kiwango cha kawaida cha kushindwa kwa kila zao litokalo kiwandani.
Nina hakika viongozi wa dini wangepinga kipengele kinachosema kuondoa vizuizi katika upatikanaji na makatazo ya usambazaji wa vidhibiti mimba; kwani viongozi wa dini wanazuia matumizi ya vidhibiti mimba kutokana na madhara yake kwa watumiaji – kama vike kusababisha saratani ya matiti, saratani ya mlango wa tumbo la kizazi, magonjwa ya moyo, kupofuka macho, kuharibika mwenendo wa hedhi, kusababisha utasa wa muda au wa kudumu. Ni viongozi wa dini wasioruhusu vidhibiti mimba kusambazwa katika vituo vyao vya afya. Pia viongozi wa dini wangelalamika kuwa matumizi ya vidhibiti mimba yanachangia uasherati miongoni mwa watu wa ndoa, watu wasio na ndoa na zaidi sana miongoni mwa wasichana. Matumizi ya vidhibiti mimba yanahusishwa na kuvunjika kwa ndoa, kumomonyoka maadili na watu kumwasi Mungu.
Viongozi wa dini wangelaani kipengele kinachozungumzia adhabu kwa mhudumu wa afya anayefanya kinyume na msukumo wa matumizi na usambazaji wa vidhibiti mimba kwa sababu kila mtu ana haki juu ya kufanya au kutenda kulingana na dhamiri yake. Mhudumu wa afya Mkatoliki, au hata Mkristo mwingine yeyote atapinga matumizi ya vidhibiti mimba kwa sababu kwanza anafahamu madhara ya vidhibiti mimba kutokana na taaluma yake; pia atapinga matumizi ya vidhibiti mimba kwa sababu yanapingana na mafundisho ya kanisa; na hatimaye angepinga kwa sababu yanakiuka misingi ya dhamiri, kwani kama mtu anaona vitendo fulani kuwa vibaya, sio vema kumlazimsha kuvitenda
Viongozi wa dini watashangaa kuyafanya mashirika au taasisi za kutetea uhai na familia pamoja na makanisa zifyate mkia, kwa sababu mswada unasema lazima serikali iondoe vipingamizi vya matumizi ya vidhibiti mimba ikiwemo pamoja na vizuizi vya kisheria na vizuizi katika kusambaza habari kuhusu vidhibiti mimba. Hapa ndipo unapolala utashi wa wale walioandika mswada huu, kwamba lengo lao sio “kupanga uzazi”, bali kukausha vizazi. Kama lengo lao lingekuwa jema, wasingediriki kusema kwamba serikali iwazuie wale wanaosema ukweli kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya vidhibiti mimba. Viongozi wa dini wangelalamika kwa kufanywa kuwa maadui wao wakubwa. Kwani ni wao ndio wanazuia usambazaji wa vidhibiti mimba katika mahospitali na vituo vya afya vilivyo chini yao. Ni viongozi wa dini ndio wanaofundisha kuwa ni dhambi kutumia vidhibiti mimba.
Nadhani pia viongozi wa dini wangeshangaa kusikia eti kuna haki za kibinafsi na faragha katika kupatiwa huduma za uzazi wa mpango. Wangeuliza maswali mengi; kwa mfano, kama linalofanyika ni jema, kwa nini lifanyike kwa usiri na faragha kubwa. Huduma gani za uzazi wa mpango zinazotolewa kwa faragha? Faragha kwa nani? Nani anafichwa na kwa malengo gani? Viongozi wa dini wangeweza kuviona vitendo vya aina hiyo kuwa ni viovu, ndiyo maana uovu huo lazima ufichwe. Ni ajabu kubwa iliyoje, kuwa serikali isimamie programu ambazo kwa asili yake ni mbovu kwa watu wake?
Viongozi wa dini wangeunga mkono Sehemu ya III inayohusu afya ya mama wajawazito na watoto wachanga isipokuwa wangeshauri;
Huduma kwa mama mjamzito zizingatie pia huduma kwa mtoto aliyemo tumboni mwake, siyo kutoa huduma kwa yule aliyezaliwa tu, kwani kabla ya kuzaliwa mtoto huyo alikuwa akiishi ndani ya tumbo la mama yake
Kama adhabu inatolewa kwa mhudumu wa afya mzembe aliyesababisha kifo cha mama mjamzito au mtoto mchanga baada ya kuzaliwa, adhabu pia itolewe kwa uzembe wa mhudumu wa afya atakayesababisha kifo cha mtoto kabla ya kuzaliwa au kwa mhudumu au mtu yeyote akayesababisha kifo cha mtoto kabla ya kuzaliwa
Hospitali, vituo vya afya na kiliniki zitakazojengwa nchi nzima vitumike kwa ajili ya huduma za kweli za wanawake na watoto; kamwe visitumike kama vituo vya kutolea mimba kwa njia za kikemikali au upasuaji; wahudumu wa afya watakaopata mafunzo wasitumike kwa ajili ya kuua binadamu ambao wameapa kuwahudumia, wawe wale waliozaliwa au wale wasiozaliwa
Sehemu IV inayohusu afya ya ujinsia na afya ya kizazi kwa wasichana ingepata upinzani mkubwa kutoka kwa viongozi wa dini kwa sababu;
Wangeishangaa kutengeneza vyombo vya kuwezesha upatikanaji wa vidhibiti mimba kwa watoto wadogo waliomo mashuleni wa umri kati ya miaka 11 hadi 19 kwani hivyo ni vitendo vya ukiukaji wa haki ya msingi ya mtoto ya kupata elimu. Katika umri huu watoto wote, wavulana kwa wasichana, wanastahili kupata elimu kama maandalizi kwa maisha yao ya baadaye. Viongozi wa dini wangeishangaa serikali inayohamasisha vitendo vya ngono kwa watoto wa umri huu. Viongozi wa dini wangehisi kuwa hapa kuna hila za kuharibu maadili ya watoto na kuharibu kizazi chao. Na kwa kadiri vidhibiti mimba vinavyotumika katika umri mdogo ndivyo hivyo inavyokuwa rahisi kuwaharibu watoto hao kiafya na kielimu na hivyo kutengeneza taifa la watu maskini zaidi.
Viongozi wa dini wangekemea vikali pendekezo la kuwaondolea wazazi wajibu na mamlaka wa malezi ya watoto wao katika umri wa ukuaji wa watoto wao. Wangejiuliza kwa nini wazazi wasiwe na mamlaka kwa watoto wao? Je, huko siyo kuvunja mila na desturi zetu katika kupasisha malezi bora kwa watoto wetu?
Viongozi wa dini wangelaani kuwalazimisha watoto kuingizwa katika vitendo vya ngono kwa kisingizio cha huduma za afya ya ujinsia na kizazi kwa dhana za upekee na ufaragha. Watoto wapate huduma za afya ya kizazi na ujinsia kwa faragha… wakimficha nani? Je siyo kwamba kwa kufanya hivyo tunawahimiza watoto wetu kujiingiza katika vitendo vya ngono katika umri mdogo na hivyo kuchochea mimba za utotoni na vitendo vya kutoa mimba. Huko Uingereza ambako waliteremsha umri wa watoto kutumia vidhibiti mimba hadi miaka 9 wameshuhudia kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa, mimba za utotoni na vitendo vya kutoa mimba. Licha ya hayo madhara ya vidhibiti mimba, yakiwemo yale ya saratani ya matiti na shingo ya uzazi yameshamiri miongoni mwa wasichana hao.
Viongozi wa dini wangechukizwa mno na pendekezo la kutolewa adhabu kwa wahudumu wa afya wanaowashauri watoto kutojiingiza katika vitendo vya zinaa au kama watawanyima watoto huduma za uzazi wa mpango
Nadhani viongozi wa dini wangegundua kuwa kipengele hiki kinadhamiria kuharibu tabia nzuri za watoto wetu, tabia zilizojikita katika heshima na adabu kwa tendo la ndoa. Bila shaka viongozi wangependekeza kuondolewa kwa kipengele hiki au kama ingekuwa lazima kibakizwe, basi wangeshauri watoto wafundishwe stadi za maisha za kujitambua, kujikubali na usafi wa moyo ambapo tunu za kujishinda, kujiheshimu, adabu nje, utii, uvumilivu, nidhamu na upendo wa kweli vingehimizwa.
Sehemu hii ya V inayohusu kutoa mimba sio tu kwamba ingepata upinzani, bali ingelaaniwa kabisa na viongozi wa dini kwa sababu;
Wakati katiba ya nchi katika ibara ya 14 inatamka wazi haki ya kila mtu kuishi na kupata kutoka jamii hifandhi ya maisha yake, sehemu hii ya mswada inapingana kabisa na ibara hiyo ya katiba kwa kupendekeza itungwe sheria ya kuua watoto kabla hawajazaliwa. Na tena sehemu hii inapingana na sheria ya kanuni za adhabu sehemu ya 150 ambayo inamtia hatiani mwanamke anayejaribu kutoa mimba; sehemu ya 151 ambayo humtia hatiani mtu anayemsaidia mwanamke kutoa mimba; na sehemu ya 152 inayomtia mtu hatiani kwa kutengeneza au kutumia vifaa vinavyoweza kutumika kutoa mimba na adhabu zinazostahili zimependekezwa kwa kila mwenye kuvunja kanuni hizo za adhabu. Sehemu ya 219 ya sheria hii ya kanuni za adhabu imesema kwa ukali zaidi kwamba kama mimba inayotolewa imefikisha umri wa miezi 7 basi huyo mtoaji mimba atakuwa na hatia ya kuua mtoto ambaye angezaliwa na kuishi kwa kujitegemea nje ya mama na adhabu kali imewekwa kwa kitendo hicho kibaya
Kwa hakaki kama viongozi wa dini wangeelezwa vizuri sehemu hii wasingekubali kabisa, na nadhani wangeususia mkutano huu kwa kubaini kuwa wamedanganywa na wameshirikishwa katika masuala ya mauaji ambayo mwasisi wake ni Ibilisi/Shetani. Viongozi wa dini wanajua kuwa Shetani ni muongo na mwuuaji tangu kale, litokalo mdomoni mwake ni uongo na sauti yake ni mauaji. Anafurahia kuona binadamu mdogo anauawa kwani yeye hujilisha na hujishibisha katika damu ya watoto hao.
Viongozi wa dini wangeshangaa kushirikishwa katika kutunga sheria ya kuwaua watoto kabla ya kuzaliwa kama uwepo wa watoto hao katika matumbo ya mama unahatarisha afya ya mama huyo kimwili na kiakili; kama kuna uwezekano wa kuzaliwa mtoto mlemavu; au kama mwenye kubeba mimba ni mama mwenda wazimu. Viongozi wa dini wanafahamu kwamba kila mama mja mzito hupitia vipindi vya mabadiliko ya kimwili na kiafya, na hiyo ni hali ya kawaida kwa kila mwanamke na huondoka yenyewe kwa kadiri mimba inavyokuwa kubwa; kila binadamu ana mapungufu yake kimwili na kiakili, na hii ina maana kuwa kila binadamu ni mlemavu. Hata tu kwamba mtu amekaa chini akaandika mswada wa kuwaua watoto walemavu ni ulemavu wa aina yake, kwani silika ya binadamu ni kumpenda binadamu mwingine kama ambavyo yeye angependa kutendewa. Kila binadamu ameumbwa kwa makusudio fulani, na katika kutekeleza hilo Mungu amemwumba kila mmoja tofauti na mwenzake. Ndiyo kusema kila ulemavu unakusudio maalumu na Mungu. Kwa miaka michache ya nyuma Visiwa vya Comoro vilikuwa chini ya utawala wa mtu mwenye ulemavu wa ngovi, albino. Je kama angeuawa wangempata wapi rais wa aina hiyo. Walemavu wamefanya mambo ya kushangaza na kuufaidisha ulimwengu katika historia ya uumbaji wa Mungu. Ni kweli mwanamke anaweza kuwa mwenda wazimu, lakini kwa nini utunge sheria ya kumwua mtoto wake badala ya kumpatia mwanamke huyo huduma nzuri ili ajifungue salama? Mbona kuna vituo vingi vya kulelea watoto; hivi kwa nini mswada ufikirie kumwua mtoto wa mwenda wazimu badala ya kufikiria namna bora ya kuwahudumia watoto wa mama huyo.
Ingekuwa katika nchi za Ulaya, Marekani au kwingineko, kama mtu au taasisi inapendekeza sheria inayopingana na katiba ya nchi zao, bila shaka mtu huyo au taasisi hiyo ingeonekana kuwa ya kigaidi na angetendewa kama mhaini. Soma sehemu ya tano ya mswada huu ambapo sehemu ya kwanza (20;1) mwandishi anatambua kuwa vitendo vya utoaji mimba katika nchi yetu ni vya kuvunja katiba na bado mwandishi huyo, bila aibu anasema, hata kama nchi yenu hairuhusu utoaji mimba, lazima itungwe sheria ya kutoa mimba(21;1-5). Viongozi wa dini wangejiuliza, jee ‘huyu ni mwenzetu’? Na viongozi wa dini sio wajinga, wanajua kuwa sheria za kutoa mimba katika nchi za Kiafrika zinasukumwa kwa nguvu na watu wa nchi za magharibi wakitumia mashirika yao, kama vile Care International na White Ribbon Alliance. Na wanasukuma kwa nguvu hivi kiasi kwamba wanataka kila nchi ya kiafrika iwe imetunga sheria za kuua watoto wao ambao hawajazaliwa kama sharti la kufikia malengo ya milennia. Viongozi wa dini wanaelewa pamekuwepo na msukumo katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Msumbiji, Zambia, Namibia, Lesotho, Botswana na hata huko Nigeria. Kwa hiyo msukumo unaofanyika hapa Tanzania ni msukumo wa kiulimwengu ulioasisiwa na nchi za Magharibi ambazo zenyewe zimepukutika kiidadi kiasi kwamba zinakosa nguvu za kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Silaha pekee iliyobaki ni kuzikandamiza na kuzidhohofisha nchi za Afrika ili kwa kadiri zitakavyopukutika ndivyo hivyo wao watakuwa na uwezo kuzitawala kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Waafrika wanaelewa jinsi walivyodhohofishwa kutokana na kununuliwa na kutumikishwa katika biashara ya utumwa na hali hiyo ilifanya zoezi la kutawaliwa liwe jepesi. Waafrika wanajua jinsi walivyotawaliwa kisiasa na kimabavu, wakabaki kuwa watwana katika nchi zao. Waafrika wanajua jinsi, baada ya uhuru wa kisiasa nchi za magharibi zilivyoendelea kuwanyonya kiuchumi na kutawaliwa kiakili. Waafrika wanafahamu yote hayo. Leo, kwa kuwatumia Watanzania wenzetu wenye uchu wa kujinufaisha kibinafsi, wanataka kutuingilia hata kitandani na kutuamulia juu masuala ya uzazi wetu. Hayo ni matusi makubwa. Viongozi wa dini hawawezi kukubali matusi haya, lazima wayakatae, lazima waukatae mswada huu. Hawawezi kukubali nchi yao iwe shamba la kumwagia damu za watoto wachanga ambao bado hawajazaliwa
Viongozi wa dini wanafahamu kuwa vitendo vya kutoa mimba vina uhusiano mkubwa na kafara za kipagani zilizotolewa kwa ajili ya kufurahisha maumbile, hizo zilikuwa enzi za upagani. Leo hii, viongozi wa dini hawawezi kukubali kurudi katika upagani wa kutoa kafara za damu za watoto wa Kitanzania ambao bado hawajazaliwa. Kufanya hivyo ni kukubali kuwa tunaanza safari ya kumaliza vizazi vya baadaye vya taifa hili. Watu wa Magharibi wamefikia hapo kwa gharama kubwa. Ndiyo maana huzuni na kukata tamaa kumetanda miongoni mwa watu wao; usishangae unapoona kushamiri kwa vitendo vya ushoga na umame. Ni matokeo ya jamii iliyomwasi Mungu na kumkumbatia Shetani.
Sehemu ya VI inayohusu virusi vya ukimwi na ukimwi na magonjwa ya zinaa isingekuwa na vipingamizi kutoka kwa viongozi wa dini. Nadhani wangependekeza njia sahihi na za kudumu za kuangamiza janga la ukimwi na kufutilia mbali maambukizo ya magonjwa ya zinaa; njia ambazo wangependekeza zingekuwa zifuatazo:
Elimu sahihi ya ujinsia wa binadamu; ambapo mtu angefundishwa kuuthamini ujinsia wake na kuutunza dhidi ya uharibifu
Elimu ya usafi wa moyo; ambapo wanafunzi na wakubwa wangeelimishwa umuhimu wa kubaki waaminifu katika maisha kabla na baada ya ndoa
Wangeshauri kutojihusishwa na vitendo vya ngono kwa njia yoyote ile, kwani vitendo hivyo ndiyo njia kuu ya maambukizo ya virusi na magonjwa ya zinaa
Wasingeshauri matumizi ya kondomu kwani wanafahamu kuwa kipo kiwango cha kushindwa cha asilimia kati ya 10 na 15 kwa watumiao kondomu
Ujumbe wa viongozi wa dini katika kudhibiti maambukizo ungekazia stadi za maisha za kujishinda, kujiheshimu na kazingatia mahusiano yenye manufaa katika maisha
Njia sahihi ni ile inayolenga katika kufuta kabisa maambukizo na sio kupunguza maambukizo
Mila potofu zinazoathiri afya ya ujinsia na afya ya kizazi ndiyo sehemu ya VII ya mswada huu. Viongozi wa dini wangewashangaa watoaji mada kwa sababu zifuatazo:
Inakuwaje ukeketaji uonekane ni mila potofu na kufunga kizazi na utoaji mimba vionekane ni vitendo vizuri. Wanafahamu wazi kuwa ukeketaji unahusu kukata sehemu ya kiungo cha uzazi cha mwanamke. Lakini wangeshangaa, kama ukeketaji ni mbaya kwa vile mwanamke anakatwa sehemu ya kiungo cha uzazi, inakuwaje vitendo vya kufunga kizazi viwe vizuri ambavyo siyo tu inakata mirija ya uzazi lakini inamfanya mwanamke kuwa tasa maisha yake yote. Wangeshangaa pia kuona kuwa ukeketaji unapigiwa kelele wakati hao hao wanapendekeza kutungwa sheria ya kutoa mimba, ili hali wanafahamu kuwa katika kila tendo la utoaji mimba mwanamke anajeruhiwa katika viungo vya uzazi na mtoto wake anauawa. Matokeo mawili kwa wakati mmoja; mwanamke kuumizwa kutokana na kuingizwa vyuma na mtoaji mimba anayetumia nguvu, na mtoto wa mwanamke huyo kuuawa. Kama ukeketaji ni mbaya, vitendo vya kufunga kizazi na kutoa mimba pia ni vibaya, na vyote vipigwe marufuku. Viongozi wa dini wangeshangaa; je ukeketaji ni mbaya kwa sababu ilikuwa sehemu ya mila za Mwafrika? Na je, vitendo vya kufunga kizazi na utoaji mimba vinakuwa vizuri kwa sababu vimeletwa kwetu na watu wa magharibi?
Tunawashangaa waandishi wa mswada wanasema eti kuna miiko mibaya katika vyakula. Mbona wao wanasema watashughulikia miiko inayozungukia vitendo vya utoaji mimba; yaani wanataka watu waone vitendo vya utoaji mimba kuwa ni vya kawaida tena vizuri na kila mmoja afanye. Kwetu sisi utoaji mimba ni mwiko mkubwa katika jamii. Na viongovi wa dini wanafundisha kuwa kutoa mimba ni dhambi ya mauti na mahali pa huyo mtoaji mimba ni makao katika moto wa milele. Hebu fikiria kosa la kuua watoto wasiozaliwa – hujui unaweza kumwua rais wa kesho, daktari bingwa, mwalimu, waziri mkuu na wengine wengi
Kama mswada unapendekeza kuendesha kampeni za kielimu juu ya vitendo viovu, viongozi wa dini wangeshauri, kampeni hiyo ihusu pia elimu kuhusu madhara ya vidhibigi mimba na utoaji mimba na madhara ya kufunga kizazi
Sehemu ya VIII inayohusu kuundwa mahakama ya kuwashughulikia masuala haya, naamini viongozi wa dini wangekataa na kushauri zifanyiwe marekebisho sheria zilizopo ili kukidhi hayo mapungufu. Viongozi wa dini wangesema pia kuwa, ili sheria mpya itungwe, basi kwanza katiba ifanyiwe marekebisho. Hata hivyo marekebisho hayo yawe yenye manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
HITIMISHO
Nadhani viongozi wa dini mlioshiriki mkutano huo mmedanganywa nanyi mkadanganyika. Mliyoambiwa siyo yale mliyotakiwa mwambiwe. Jiondoeni katika mtego huo wa kishetani. Kama mlipokea fedha za kuwanunua ili mkubaliane na mswada huo, rudisheni. Kama hamtaki, vueni mavazi yenu yanayowatambulisha kama viongozi wa dini ili muwe waamini wa kawaida. Angalieni msije kuwa sababu ya kilio cha Watanzania. Mungu atawahukumu mbele ya haki.