MSWADA WA SHERIA YA UZAZI SALAMA (2012): Kilio na majonzi kwa Watanzania
Lipo shirika la nje ambalo linasukuma sheria inayodaiwa kulinda haki za wanawake waja-wazito na wasichana katika kuzifikia huduma za “afya ya kizazi”. Tayari muswada wa sheria hiyo utawasilishwa kwa kikundi cha Wabunge mwezi huu [Februari] ili kuanzisha mchakato wa kutungwa sheria hiyo. Akiwasilisha muhutasari wa muswada huo, mwakilishi wa shirika hilo anasema kuwa lengo la sheria hiyo itakayojulikana kama “Safe Motherhood Law (2012)” ni kulinda haki za wanawake waja-wazito, wasichana na wavulana za kupata huduma za ‘afya ya kizazi’
Mchakato huu ulianza Juni mwaka jana ambapo ilikubalika haja ya kutunga sheria itakayolinda haki za mama waja-wazito dhidi ya vifo vitokanavyo na uja-uzito na vifo vya watoto wachanga. Kwa kadiri ya msemaji wa shirika hilo, sheria hiyo itakuwa na vipengele vingi vinavyohusu upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango kwa njia ya vidhibiti mimba, afya ya mama mzazi na watoto wachanga na afya ya ujinsia na afya ya kizazi kwa wasichana na wavulana. Vingele vingine katika muswada huo vinahusu utoaji mimba, UKIMWI, magonjwa ya zinaa, vitendo potofu vinavyoathiri afya ya ujinsia na afya ya kizazi ambapo kanuni zitatungwa za kuhakikisha utekelezaji wake. Tunaelezwa kuwa muswada huo unachangiwa na hali kwamba sheria za sasa kuhusu maeneo hayo, kama vile sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ina mapungufu mengi. Sheria nyingine zilizotajwa kuwa na mapungufu ni; Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009, na Sheria ya Wafungwa ya mwaka 1967.
Kwa kadiri ya msemaji huyo, nchi kama Benin, Chad, Mali, Ufilipino na Afrika ya Kusini tayari zina sheria hiyo na utafiti wa jumla unaonyesha kuwa yapo mafanikio katika upatikanaji wa huduma za afya ya ujinsia na afya ya kizazi. Mbunge Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge kuhusu uzazi salama alisema, sheria hiyo ni muhimu ili kulinda uhai wa mama na mtoto.
Napenda kuwajulishe Watanzania kuwa jitihada hizi sio mpya, ni jitihada zilezile zinazokusudia kuhakikisha kwamba vizazi vya Watanzania vinaporomoka kwa njia ya vidhibiti mimba, utoaji mimba na mengi mengineyo yanayofanana na hayo. Nchi za Magharibi na Mashirika yao yanaona ukuaji wa idadi ya watu katika nchi zinazoendelea kuwa ni tishio kwa maslahi yao kiuchumi na kisiasa. Kupomoroka kwa vizazi kulikozikumba nchi za Magharibi kwa sasa kumeleta zimanzi kwa serikali za nchi hizo. Kukua kiuchumi kwa nchi za Mashariki, ikiwa ni pamoja na China na nchi za Mashariki ya Kati, kama vile Iran kunaonekana kuwa tishio kwa nchi za Magharibi. Wimbi la maasi linalozikumba nchi za magharibi, kama vile kule Marekani, Uingereza, Ufaransa na kwingineko kunaleta kero kwa watawala wanaoona kuwa vitendo hivyo vinachochewa na uhamiaji wa watu kutoka nchi zinazoendelea. Huko nyuma nchi hizo zilielekeza nguvu katika kudhibiti idadi ya watu katika nchi zinazoendelea kwa maelezo kuwa watu wanaoongezeka watakuwa chanzo cha ghasia, uhalifu na ugaidi duniani. Hata kuibuka kwa mapinduzi katika nchi za Kiislamu duniani, kwa upande mmoja unaweza kutafsiri kuwa ni jitihada za watu kutaka utawala bora; kwa upande mwingine kunaweza kutafsiriwa kuwa ni jitihada za nchi za magharibi katika kuzidhohofisha nchi hizi ambazo zinaonekana kufanya vizuri katika midani za kiuchumi na kisiasa.
Watanzania wenzangu, hebu niwasaidieni uelewa wa dhana za “afya ya ujinsia” na “afya ya kizazi”. Naelewa kuwa, katika mswada huo waandishi wametafsiri dhana hizo ili kukidhi madhumuni yao. Lakini mimi nawaletea tafsiri yetu kwa mtazamo wa utetezi uhai. Mnaposikia maneno “afya ya ujinsia kwa vijana” ina maana ya kuwapatia vijana wetu nyenzo – kondomu – ili wafanye “ngono salama”, maana yake wasipate mimba na magonjwa ya zinaa. Na wanajua fika kuwa matumizi ya kondomu, licha ya viwango vyake vya kushindwa, yanatimiza lengo kuu moja: kuzuia uzao. Kwa hiyo, kadiri vijana wanavyotumia kondomu, ndivyo hivyo inakuwa rahisi kudhibiti vizazi vyao. Lakini wanajua tena kuwa kuhimiza matumizi ya kondomu kwa vijana ni kuhimiza vitendo vya ngono – uasherati – miongoni mwa vijana.Dhana ya “afya ya kizazi” humaanisha matumizi ya vidhibiti mimba, kufunga kizazi na utoaji mimba. Kwa nini mkazo unawekwa kwa vijana(hasa wasichana; na kwa kweli neno ‘wavulana’, nadhani limewekwa kwa bahati mbaya) ni kwa sababu wanajua vidhibiti mimba vitaharibu vizazi vya vijana kiasi kwamba watakapofikia umri wa kuwa na ndoa au kuzaa, baadhi yao watashindwa kupata uja-uzito; wengine watakuwa wamedhohofika kiasi kikubwa na hivyo kutoshauriwa kuzaa. Programu ya kuwafunga kizazi vijana ni programu ya kishetani, kwani hatima yake ni kufutilia mbali kizazi kijacho cha taifa letu. Vijana wakihamasishwa kufanya ngono, basi inakuwa rahisi kwao kupata mimba za utotoni, wakiwa bado shuleni na hivyo litakalofuata ni kufungua vituo vya kutolea mimba ili kuwawezesha vijana kutimiza malengo au ndoto zao. Kwa hiyo utoaji mimba ni vitendo vinavyofuatia matumizi ya vidhibiti mimba.
VIPENGELE VYA MUSWADA WA SHERIA YA “UZAZI SALAMA”
THE BILL ON SAFE MOTHERHOOD (2012)
Mswada una sehemu kuu 8:
Sehemu ya 1 inahusu maelezo ya awali ambapo unasema Sheria itaitwa “Safe Motherhood Act, 2012” na itaanza kutumika siku ambapo Waziri anayehusika na masuala ya afya atatoa tangazo katika gazeti la serikali; na kwamba sheria hii itahusu Tanzania Bara tu; na kuna tafsiri ya dhana mbalimbali. Kwa mfano, afya ya ujinsia, afya ya kizazi,kutoa mimba – ina maana ya kutenganisha na kutoa nje, kunakofanywa na daktari, vitu vilivyomo tumboni mwa mama mja mzito.
Sehemu ya 2 inahusu upatikanaji wa vidhibiti mimba na uzazi wa mpango; ambapo tunaambiwa kuwa serikali itahakikisha kwamba kila mtu binafsi atakuwa na haki ya kudhibiti kizazi chake kwa kutumia vidhibiti mimba na kwamba serikali itatoa huduma ya uzazi wa mpango na kwamba yeyote atakayeweka vizuizi katika matumizi ya vidhibiti mimba atachukuliwa hatua kali za kisheria
Sehemu ya 3 inahusu uzazi salama na kuwataja watakaohusika na utoaji wa huduma hiyo
Sehemu ya 4 inahusu afya ya ujinsia na afya ya kizazi kwa wasichana [na wavulana]; ambapo inaelezwa kuwa watoto watapata huduma za uzazi wa mapango bila kulazimika kupata ridhaa ya wazazi na vipingamizi vyote vinavyowanyima wasichana kutumia uzazi wa mpango vitaondolewa na itakuwa jukumu la serikali kugharamia huduma hizo
Sehemu ya 5 inahusu utoaji mimba ambapo mswada unasema kuwa uamuzi wa kutoa mimba utahusu mwenye mimba na mtoa huduma hiyo na kwamba vituo maalumu vitatengwa kwa ajili hiyo na kwamba wizara husika itateua vituo vya afya vya kutolea ushauri nasaha kwa wanawake watakaopata madhara baada ya kutolewa mimba; mhudumu wa afya atapata adhabu kali kama atakataa kumtoa mwanamke mimba
Sehemu ya 6 inahusu UKIMWI na magonjwa ya zinaa
Sehemu ya 7 inahusu matendo mabaya yanayoathiri afya ya kizazi; ambapo baadhi yake vinatajwa kuwa ndoa za utotoni, mke kurithiwa, miiko katika vyakula na kwamba adhabu kali itatolewa kwa mtu yeyote atakayefungisha ndoa za utoto, yaani kama msichana hajafikisha umri wa miaka 18
Sehemu ya 8 inahusu utekelezaji wake na vyombo vitakavyoundwa ili kusimamia utekelezaji wake na majukumu ya kila chombo.
Ndugu Watanzania, kama mswada huu utapitishwa na Bunge letu na Rais kuusaini na kuwa sheria, basi tufahamu kuwa Tanzania itakuwa nchi ya kwanza dunianikutunga sheria kandamizi kwa watu wake kuliko nchi yoyote duniani.
Sheria itakiuka sheria mama – yaani KATIBA ya Jamhuri ya Mwungano wa Tanzania inayotamka wazi katika ibara ya 6 haki ya kuishi na wajibu wa jamii kuheshimu na kuweka mazingira ya kulinda haki hiyo
Itakiuka misingi ya maadili ya kiutamaduni juu ya malezi ya watoto wetu
Itadhalilisha sheria na taratibu za kidini juu ya ndoa
Itafuta sheria zote za nyuma zinazolinda uhai na afya za binadamu na kufanya matumizi ya vidhibiti mimba na utoaji mimba kuwa jambo la lazima kwa kila mtu.
Itakiuka kanuni ya kuheshimu dhamiri na uhuru wa mtu wa kuzungumza na kutoa maoni kwa kutoa adhabu kwa mtu atakayeeleza ubaya wa vidhibiti mimba na mhudumu wa afya anayekataa kumtoa mwanamke mimba
Inajipinga; kama mtoto wa miaka 11 anawekwa huru kutumia vidhibiti mimba, inakuwaje sheria hiyohiyo imkataze kuolewa kabla ya miaka 18? Ni wazi sheria hii itahimiza vitendo vya utoaji mimba
Itawatia hatiani wahudumu wote wa kiimani, mapadre, wachungaji, maimu/mashehe kama watafungisha ndoa wasichana walio chini ya umri wa miaka 18
Watetezi uhai na viongozi wa kiimani watatiwa hatiani kama watasema ukweli kuhusu madhara ya vidhibiti mimba na utoaji mimba
Itafanya upatikanaji wa vidhibiti mimba kuwa wa lazima kwa kila mtoto mdogo na hata bila idhini ya wazazi
Itaipa serikali mamlaka juu ya maamuzi ya kifamilia ambayo ni ukiukwaji wa haki ya faragha ya kifamilia
Itatekelezwa kimabavu
Kama tulivyosema juma lililopita kuwa sheria hii inafuata nyayo za Itifaki ya Maputo ambapo ilizitaka serikali za Afrika kutunga sheria ya kuua watoto wao kikemikali. Sheria ya sasa ni mbaya zaidi kwani imeletwa kwa lugha ya vitisho kutokana na adhabu kali zilizopendekezwa. Kama ilivyokuwa kwa Itifaki ya Maputo sheria hii imeandikwa na mashirika ya kimataifa ya magharibi yenye lengo la kuendesha kampeni dhidi ya ukuaji wa idadi ya watu nchini mwetu. Huu ni ubeberu wa kimagharibi wenye kudhaminiria kunyang’anya rasilimali zetu. Hawa wanajua kuwa hawawezi kupora rasilimali zetu kama idadi ya watu wetu itakuwa kubwa hasa kundi la vijana, kwa hiyo wanafanya kila njia kutufanya tupungue na hivyo kupunguza watu wanaoweza kufikiri na uwezo wa kujitetea.
Watetezi uhai, watu wenye imani ya kweli kwa Mungu Muumba, na watu wote wenye mapenzi mema tunasema kwa nguvu zetu zote kuwa kamwe hatutakubali sheria hii ipitishwe. Tuungane kutupitia mbali sheri ya UZAZI SALAMA, ambayo ni ulaghai wa maneno kwa jambo zito lililofichika, yaani Kuvuruga misingi mizuri ya utamaduni wetu, utaifa wetu na kumaliza kizazi cha baadaye cha taifa letu.
SEHEMU YA I
MAELEZO YA AWALI
Katika sehemu hii mswada unatoa ufafanuzi juu ya dhana mbalimbali kwa kadiri waandishi wanavyotaka zielezeke. Nitazipitia zile muhimu tu kwa kadiri ya mahitaji ya watetezi uhai.
“ujana” (adolescence) humaanisha kipindi cha kukua kimwili na kisaikolojia kutoka mwanzo wa balehe hadi kukamilika kukua na kuingia utu uzima, yaani kati ya miaka 11 hadi 19
“vidhibiti mimba” (contraception) humaanisha uamuzi wa makusudi wa kuzuia mimba kwa njia ambazo mwenendo wa asili vipindi vya uzazi huzuiwa, kuzuia kutungwa mimba na kuzuia mimba kujipandikiza
“vidhibiti mimba vya tahadhari” (emergency contraception) ni aina ya vidhibiti mimba vinavyotumiwa na wanawake mara tu baada ya tendo la kujamiiana ambalo halikuwa na kinga ili kuzuia mimba [kujipandikiza]
“kupanga uzazi” (family planning) ni jitihada za makusudi za majozi au mtu binafsi na wanawake kuamua kwa uhuru juu ya idadi ya watoto wa kuwazaa na kuweka mpishano wa uzao na muda wa kuzaa kwa kutumia au bila kutumia vidhibiti mimba
“vitendo viovu” maana yake matendo ya kidini au ya kiutamaduni ambayo huleta madhara katika afya ya ujinsia na afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana
“ukubalifu wa hiari” (informed consent) maana yake ukubalifu unaofanyika kwa uhuru bila vitisho au kulazimishwa baada ya kupata ushauri na uelewa wa taarifa za uhakika na zinazoeleweka katika muundo na lugha ya mgonjwa
“afya ya kizazi” (reproductive health) maana yake hali ya kuwa na afya kimwili na kisaikolojia na hali za kijamii katika mambo yote yahusuyo mfumo wa uzazi na utendaji wake, na siyo tu inahusu kutokuwepo magonjwa or itahira
“haki za afya ya kizazi” (reproductive health rights) zinajumuisha haki ya mtu kupata afya ya ujinsia na kizazi kwa kiwango cha juu na kufanya maamuzi kuhusu maisha yao ya kiafya, idadi na mpishano wa uzao wa watoto bila ubaguzi, kulazimishwa or kutumia nguvu
“afya ya ujinsia” (sexual health) humaanisha hali ya bora ya kimwili, kimhemuko, kiakili na kijamii yahusianayo na ujinsia
“kutoa mimba” (termination of pregnancy) humaanisha kutenganisha/kukatakata [separation] na kutoa nje [expulsion], kwa njia za kikemikali au upasuaji, kilichomo katika tumbo la mwanamke mja mzito
SEHEMU II
UPATIKANAJI WA VIDHIBITI MIMBA NA KUPANGA UZAZI
Sehemu hii [4.1] mswada unaiagiza serikali kuhakikisha haki za mtu binafsi katika kudhibiti kizazi chake, kuamua idadi ya watoto na mpishano wa uzao, kufahamishwa na kuchagua njia yoyote ya vidhibiti mimba ambavyo vinatakiwa viheshimiwe na vidumishwe. Vilevile unaiagiza [4.2] serikali kuwajibika katika kuhakikisha upatikanaji wa vidhibiti mimba na huduma za uzazi wa mpango ikijumuisha vidhibiti mimba vyenyewe, kutoa ushauri nasaha, kutoa taarifa na kutoa elimu juu ya matumizi yake.
Katika sehemu hii [5] Waziri wa Afya anaagizwa kuweka taratibu za kuhakikisha kwamba kila mhitaji anapata vidhibiti mimba vyenye hadhi ya hali ya juu, taarifa juu ya njia zinazokubalika za uzazi wa mpango na kutoa miongozo kwa ajili ya:
kuhakikisha upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango za kisasa na za asili, pamoja na vidhibiti mimba vya tahadhari
kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ushauri nasaha, habari na elimu bila kujali hali ya ndoa na umri
kulinda haki za mtu za kukubali kwa hiari kabla ya kukubali njia za vidhibiti mimba
kuhakikisha kuwa vidhibiti mimba vyote vinakidhi ubora wa viwango vya kimataifa
kujali haki ya faragha na usiri katika utoaji wa huduma za uzazi wa mpango
kuondoa vipingamizi vyote katika vidhibiti mimba ikiwa ni pamoja na vipingamizi vya kisheria na makatazo katika utoaji wa elimu kuhusu vidhibiti mimba
Mswada unasema, katika [kipengele cha 6], kuwa mhudumu wa afya anayetoa vidhibiti mimba atatoa taarifa kwa mteja apokeaye huduma hiyo kuhusu faida na hasara zake na kuhakikisha kuwa ukubalifu na usiri unazingatiwa.
Kipengele kinachofuata [7] kinasema kuwa mhudumu wa afya atakayekiuka kipengele cha 6 atakuwa ametenda kosa na kama atapatikana na hatia atahukumiwa kulipa faini isiyozidi laki tano au kutumikia kifungo kwa muda usiozidi miezi 3 au zote kwa pamoja.
Na sehemu ya mwisho [8] unaitaka Wizara kudumisha na kulinda haki za wanaume na vijana katika kupata taarifa na kuwezeshwa kupata njia za uzazi wa mpango zilizo salama, zinazowezekana na zinazokubalika kulingana na uchaguzi wao
SEHEMU YA III
UZAZI SALAMA NA AFYA YA MTOTO
Katika sehemu hii
Kipengele cha [9] kinaiagiza Wizara ya Afya kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za bure na za kiwago cha juu kwa mama na mtoto, utoaji habari na elimu ikiwa ni pamoja na:
Huduma za kabla ya uja-uzito na baada ya uja-uzito
Huduma wakati wa uja-uzito na kujifungua salama
Huduma baada ya kujifungua
Wanatajwa [10] watu wanaoruhusiwa kutoa huduma ya uzazi
Madaktari
Waganga wasaidizi
Wakunga
Wizara [11.1] inatakiwa kuimarisha uwezo wa Bodi za Afya ili kuhakikisha kuwa utolewaji wa huduma hizo kwa mama na mtoto zinakuwa za kiwango cha juu. Na katika [11.2] mswada unamtaka Waziri kwa kushirikiana na Bodi za Afya kuweka kanuni ili:
Kudumisha ubora wa huduma za mama na mtoto
Kusajili na kutoa leseni kwa vituo vya huduma za afya na wahudumu wa afya
Kufanya ukaguzi katika vituo vya afya ili kuhakikisha na kulinda ubora wa huduma zitolewazo
Kutoa miongozo kwa vituo vya kufanya hesabu za watoto wazaliwao na uhakiki wa vifo vitokanavyo na vizazi
Ili kufikia azma hiyo, [12] serikali italazimika
Kuhakikisha kwamba kila kijiji kina zahanati, kila kata inakuwa na kituo cha afya na kila wilaya inakuwa na hospitali
Kuajiri wakunga wa kutosha ili kufikia walao wastani wa mwisho wa mkunga mmoja kwa kila mama wazazi 5 kwa siku
Kuhakikisha kwamba vituo vya afya vina wahudumu wa kutosha na wenye uwezo, vifaa vya kutosha na vifaa vya kuhudumia shida za dharura za uzazi
Wizara [13] inatakiwa kugharamia programu maalumu zinazowashirikisha wanaume katika maeneo yote ya uzazi na huduma za afya ya kizazi
SEHEMU IV
AFYA YA UJINSIA NA KIZAZI KWA VIJANA
Katika kipengele cha 14.1 mswada unaitaka Wizara kwa kushirikiana na bodi nyingine za afya na wizara zinazohusiana nazo kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya ya ujinsia na afya ya kizazi zenye kukidhi mahiaji ya vijana, pamoja na habari na elimu
Katika kutoa huduma za afya ya ujinsia na kizazi kwa vijana [14.2]
Kibali cha wazazi hakitakuwa hitaji la lazima
Kanuni za kutobagua, upekee na usiri zitazingatiwa
Vipingamizi vyote vya kisheria na taratibu zinazohusu afya ya ujinsia na kizazi zitaondolewa
Katika 14.3 mswada unatamka kuwa mhudumu wa afya atakayekiuka kipengele cha 14.2 atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atahukumiwa na kulipa faini isiyozidi shilingi laki tano au kifungo kwa muda usiozidi miezi mitatu au vyote viwili kwa pamoja
Serikali, kwa kadiri ya mswada, inaagizwa
kulipia gharama na kuwezesha kupatikana kwa huduma za elimu ya afya ya ujinsia na kizazi kulingana na umri wao kwa wale walio mashuleni na wale walio nje ya shule na kutolewa na walimu waliofundishwa vyema
kugharamia programu za pekee kwa ajili ya kupunguza mimba za utotoni na matatizo mengine ya afya ya kizazi kwa watoto
kulipia programu za afya ya kizazi kwa watoto wenye makundi maalumu, kama vile watoto wa mitaani, walio nje ya shule na wale waliotelekezwa
kuwalinda watoto kutokana na aina zote za uonevu wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na kubakwa, kuingiliwa na ndugu na kuuzwa
Wizara inatakiwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya vidhibiti mimba na uzazi salama, pamoja na huduma za uja-uzito kabla na baada ya kujifungua kwa vijana bila kujali kama wameolewa au la
SEHEMU YA V
UTOAJI MIMBA
Katika 17.1 waandishi wa mswada wanasema mimba inaweza kutolewa iwapo mhudumu wa afya, baada ya kushauriana na mwanamke mja-mzito, anaona kuwa
kuendelea kuwepo kwa mimba kunaweza kumletea mwanamke hatari au majeraha ya kiafya kimwili au kiakili
ipo hatari kubwa kwamba mimba itadhurika kutokana na ulemavu wa kimwili au kiakili
mimba imetokana na ubakaji au mimba ya ndugu
mwanamke mja-mzito kutokana na hali yake ya ulemavu wa kiakili, hawezi kuwa na uwezo wa kuthamini mimba aliyonayo
Sehemu ya 17.2 mswada unasema utoaji wa mimba utafanywa na mhudumu wa afya aliyepata mafunzo kwa ajili hiyo au yule mwenye cheti
Mswada unasema katika 17.3 kuwa utoaji mimba utafanyika katika kituo cha afya kilichoteuliwa na Waziri kwa kutoa tangazo katika gazeti la serikali kwa ajili hiyo
Na katika 17.4 mswada unasema Waziri anaweza kuteua kituo chochote kwa ajili hiyo, baada ya kutafakari sehemu ya 17.1, ili mradi anaona kwamba mazingira na mahitaji yanakidhi lengo la Sheria hii
Waziri, mswada unasema katika 17.5, anaweza kufuta uteuzi uliofanywa kwa kutoa notisi ya siku 14 katika gazeti la serikali
Serikali inaagizwa na mswada katika 18 kuwa ni lazima kuweka kanuni zisizolazimasha juu ya kutoa ushauri nasaha, kabla na baada ya mimba kutolewa
Mswada unasema katika 19 kwamba kulingana na 17.1 utoaji wa mimba utafanyika baada ya uelewa na ukubalifu wa mwanamke mja-mzito
Kulingana na kifungu cha 19.1, katika mazingira kuwa mwanamke hawezi kutoa ukubalifu, utoaji mimba utafanyika utaruhusiwa baada ya kushauriana na mlezi, mwanasheria mshauri au mwenzi, kwa kadiri itakavyokuwa, kama atakataa kutoa ukubalifu
Katika kifungu cha 20.1, mswada unaiagiza Wizara kuhakikisha kuwa vituo vya afya vinazuia na kushughulikia madhara yatokanayo na utoaji mimba kwa kutoa huduma za kiafya baada ya utoaji mimba, ikijumuisha
tiba ya dharura zitokanazo na utoaji mimba usiokamilika au utoaji mimba usio salama
ushauri nasaha baada ya utoaji mimba kwa lengo la kupima mahitaji ya kihisia na kiafya
ushauri wa uzazi wa mpango na huduma za vidhibiti mimba baada ya utoaji mimba
huduma za rufaa zitokanazo na matatizo ya kizazi na kiafya
kuweka mahusiano ya kijumuiya kwa ajili ya kutoa msaada unaotakiwa
Katika kifungu cha 20.2 mhudumu yeyote wa afya atakayevunja kifungu cha 17, 19 na 20 atakua ametenda kosa na atahukumiwa baada ya kupatikana na hatia faini ya shilingi zisizozidi milioni moja au kifungo cha muda usiozidi miezi 6 au adhabu zote kwa pamoja
SEHEMU VI
VIRUSI/UKIMWI NA MAGONJWA MENGINE YA ZINAA
Mswada unasema katika kifungu cha 21.1 kuwa mhudumu wa afya anayemshughulikia mama mja-mzito atampatia taarifa kuhusu virusi/ukimwi, na hasa kumfahamisha kuhusu maambukizo ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Katika kifungu cha 21.2 mswada unasema kila mja-mzito na mume au patna wake wanapohudhuria kituo cha afya watapatiwa ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya ukimwi
Ukiendelea, katika kifungu cha 21.3 mswada unasema mhudumu wa afya yeyote anayemlazimisha mja-mzito kupimwa virusi vya ukimwi au anampima mtu mwingine bila ufahamu wake atakuwa anatenda kosa
Kifungu cha 21.4 kinasema matokeo ya vipimo vya virusi yatakuwa siri na yatatolewa kwa mja-mzito na mume wake au patna wake tu.
Katika kifungu cha 22 mswada unamwagiza Waziri, kwa kushirikiana na bodi za afya
kutoa kwa umma taarifa kamilifu na za uhakika za mara kwa mara kuhusu virusi/ukimwi, pamoja na namna ya kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
kuhakikisha upatikanaji na utoaji wa matibabu kwa mama na watoto walioambukizwa
kuhakikisha upatikanaji wa ushauri nasaha kwa wanawake na waume zao or mwanaume anayeambukizwa virusi au anaumwa ukimwi jinsi ya kutunza afya ya kizazi na haki zao
Kifungu cha 23.1 kinasema kila mhudumu wa afya au mtu yeyote anayemhudumia mama mja-mzito atashauriwa kufanyiwa vipimo vya virusi vya ukimwi
Katika 23.2 kila kituo cha afya kinachowahudumia wanawake waja-wazito anawajibu wa kuhakikisha
ugawaji wa mipira ya uzazi
ugawaji wa vifaa muhimu kama vile mipira ya kuvaa mikononi, miwani na magwanda
matumizi mazuri na utupaji wa vifaa vilivyotumika, kama vile, sindano, vifaa vya kupimia damu na vifaa vya damu vinavyosadikiwa kutumiwa na watu wenye virusi
Na katika kifungu cha 32.3 mtu yeyote anayekiuka sehemu za vifungu hivi atakuwa anatenda kosa na kama atapatikana na hatia atahukumiwa kulipa faini isiyozidi shilingi laki tano
SEHEMU YA VII
VITENDO VIBAYA VINAVYOATHIRI AFYA YA UJINSIA NA KIZAZI
Kifungu cha 24, mswada unatamka kwamba vitendo vyovyote vibaya kama vile ukeketaji wa wanawake, ndoa za utotoni au kulazimishwa kuolewa, mke kurithiwa na miiko katika vyakula, ambavyo vinathiri afya ya kizazi vinavyofanywa kwa sababu za kiimani au kimila haviruhusiwi kisheria.
Katika kifungu cha 25.1 mswada unakataza kuoa au kuolewa kwa mtu ambaye hajafikisha umri wa miaka 18
Na katika kifungu cha 25.2 mswada unazuia mtu yeyote kuhusika na ibada inayosadikiwa kuwa ni ndoa kwa mtu ambaye anajua kwamba umri wake ni chini ya kiwango kilichowekwa kisheria atakuwa ametenda kosa na atatiwa hatiani na kupewa faini isiyozidi shilingi elfu tano.
Katika kifungu cha 25, mswada unasema kuwa mtu yeyote atakayesaidia kuendesha ibada iliyotajwa hapo juu atahesabika kuwa na kosa
Kifungu cha 26 cha mswada kinaitaka serikali kwa kushirikiana na taasisi husika
kuendesha elimu na kampeini ili kuwajulisha watu hasara za vitendo viovu
kuelimisha watoa huduma za afya ili wakabiliane na mahitaji mahususi ya afya ya kizazi kwa wanawake walioathirika kwa vitendo viovu
SEHEMU YA VIII
MFUMO WA KISHERIA NA UTEKELEZAJI
Mswada katika kifungu cha 28.1 unaitaka Wizara kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sheria hii na itaunda bodi ya Uzazi Salama ambayo wanachama wake watakuwa
Wizara ya Afya [RCH]
Bodi ya Madawa
Chama cha Wanasheria Tanzania
Wabunge waliomo katika kamati ya Uzazi Salama
Inaweza kupendekeza wengine
Katika kifungu cha 28.2 mswada unasema, Bodi ya Uzazi Salama itakuwa yenye sifa ya kurithisha na muhuri, na kutokana na sifa hiyo inaweza kushitaki na kushitakiwa
Muswada unatamka majukumu ya bodi, katika kifungu cha 28.3 kuwa
Kuratibu utekelezaji wa sheria hii
Kwa kushirikiana na wadau wengine kufanya utafiti wa mara kwa mara katika maeneo ya afya ya kizazi na afya ya ujinsia na kuishauri Wizara mambo yanayofaa
Kupendekeza, kuandika na kuhakikisha upitishwaji wa kanuni, miongozo na sera kwa ajili ya utekelezaji wa sheria hii
Kufanya ufuatiliaji na tathmini
Ripoti za kila mwaka kuhusu huduma za uzazi, afya ya kizazi na afya ya ujinsia [MSRH]
Kukagua vifo vya kizazi
Kupendekeza mengine yafaayo
Na katika kifungu cha 29.1, mswada unasema kuwa pataanzishwa Mahakama itakayojulikana kama Mahakama ya Uzazi Salama na Haki za Kiafya
Kifungu cha 29.2 mswada unataja wajumbe wa mahakama hiyo ambao watateuliwa na Waziri
Mwenyekiti ambaye atateuliwa kwa sifa za ujuzi wake katika masuala ya Afya ya Kizazi na Afya ya Ujinsia
Mwanasheria Mkuu au mwakilishi wake
Mwanasheria mmoja kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania atakayependekezwa na Chama cha Wanasheria Tanzania
Wawakilishi watatu kutoka bodi za taaluma ya utabibu ambao ni wataalamu katika masuala ya afya ya kizazi ambao mmoja wapo atatoka katika Bodi ya Wanataaluma wa Madawa ambayo haikuwakilishwa hapo juu
Watu wawili wenye sifa na utaalamu unaohitajika kwa kutekeleza shughuli za Mahakama
Bodi itakuwa na wajumbe wasiozidi saba
Mswada unatamka katika kifungu cha 29.3 kuwa katika wajumbe wa Mahakama hiyo, walao wanne wawe wanawake
Na idadi timilifu kifungu cha 29.4 itakuwa na wajumbe watatu
Maamuzi yatatolewa kwa wingi wa kura, kifungu 29.5
Wajumbe wa Mahakama, kifungu 29.6 watalipwa mishahara na marupurupu kwa kadiri atakavyopanga Waziri kwa kushirikiana na Hazina
Ofisa mtendaji mkuu [CEO] wa Bodi, kifungu 29.7 atakuwa mjumbe asiyekuwa na haki ya kupiga kura
Katika kifungu cha 30 mswada unasema, nafasi ya mjumbe wa Mahakama itakuwa wazi
Kufikia ukomo wa huduma wa miaka mitatu tangu tarehe ya kuteuliwa kwake na ukomo wa kuteuliwa utakuwa vipindi viwili [vya miaka mitatu mitatu]
Kama mjumbe anaacha kuwa mhudumu au uganga kama ilivyoelezwa katika kifungu cha (1)
Kama mjumbe ataachishwa uanachama wa Mahakama na Waziri kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na ugonjwa wa kimwili au kiakili, au kutokana na sababu nyingine au utovu wa nidhamu, na
Kama mwanachama anajiudhuru ujumbe wa Mahakama. Ili mradi kwamba Waziri atakuwa na uhuru wa kumteua mwanachama mwingine kwa kipindi kingine, ila tu kwamba hakuna mtu atakayetumikia kwa zaidi ya vipindi viwili na kwamba Waziri anaweza kubadilisha muda wa uteuzi ili isitokee kwamba zaidi ya theluthi moja ya wajumbe wanaacha kwa wakati mmoja
Kifungu cha 31.1 mswada unataja majukumu ya kisheria ya Mahakama
Kusikiliza na kuamua malalamiko yatokanayo na uvunjifu wa kifungu chochote cha Sheri hii
Kusikiliza na kuamua masuala yoyote yale yatolewayo kuhusu Sheria hii
Kutekeleza majukumu mengine kama yatakavyotajwa na Sheria hii au sheria nyingine yoyote inayotumika
Katika kifungu 31.2 mswada unasema baada ya kusikiliza malalamiko Mahakama itakuwa na mamlaka ya kisheria na kuwaita mashahidi, kupata ushahidi baada ya kiapo au uthibitisho na kuitisha vitabu na majarida mengine
Kifungu cha 31.3 mswada unatamka kuwa Mahakama, katika siku kumi na nne baada ya kupokea malalamiko, itapeleka kimaandishi notisi ya mlalamikaji kwa mlalamikiwa ikimweleza atayarishe majibu katika siku 28 baada ya notisi
Pale mahakama itakapoona inafaa, kifungu 31.4, inaweza kupokea ushahidi kwa vielelezo muhimu na kuanzisha mahojiano na kumtaka mtu ambaye anafanyiwa mahojiano kujibu inavyopasa katika muda uliopangwa na mahakama
Katika kuangalia jambo lolote, kifungu 31.5, mahakama inaweza kutumia ushahidi mwingine wowote ambao inaona unafaa katika suala husika, hata kama ushahidi huo usingekubalika katika Sheria za Ushahidi
Kifungu cha 31.6 kinasema mahakama itakuwa na uwezo wa kuitisha ushahidi wa kitaalamu katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria hii
Mahakama itakuwa na uwezo, kifungu cha 31.7, wa kuamuru malipo katika shauri la kesi iliyoendeshwa, na kuelekeza kwamba malipo hayo pamoja na makato ya kodi, yatafanywa kwa mujibu wa viwango vya Mahakama Kuu au kufuta kutoa adhabu ya malipo ya kiwango fulani
Notisi zozote au nyaraka nyingine, kifungu 31.8, zitakazotolewa kwa mkono na mhuri wa mwenyekiti zitahesabika kama zimetolewa na Mahakama
Malalamiko yoyote yale, kifungu 31.9, yanapelekwa kwenye Mahakama kwa mujinu wa Sheria hii, Mahakama inaweza;
Kusikiliza malalamiko hayo na kuamuru kama inavyoonekana inafaa na kwa haki
Kupendekeza kufuta, kusimamisha au kufuta cheti cha mhudumu [wa afya]
Kutoa amri kulingana na mazingira husika
Katika kifungu 31.10, mlalamikaji anaweza kuwakilishwa na wakili, au mtu mwingine ambaye, mahakama, kulingana na jinsi itakavyoona inafaa, inaweza kukubali kusikiliza kwa niaba ya mlalamikaji
Kifungu cha 31.11 kinasema kuwa upande ambao haukuridhika na maamuzi ya Mahakama utakuwa na haki ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu katika siku thelathini baada ya hukumu kutolewa
32. Mtu yeyote ambaye ameitwa na Mahakama kuhudhuria na kutoa ushahidi au kuwasilisha taarifa, vitabu vya hesabu, maelezo, au nyaraka nyingine, au anatakiwa kujibu maswali ya kuhojiwa na ambaye, bila sababu ya msingi;
a) Anakataa au anashindwa kujibu, kutoa majibu yasiyo tosheleza, kwa kadiri ya ufahamu wake na kuamini kuwa maswali yote yaliyoelekezwa kwake na, au kwa kuendana na Mahakama; au
b) anakataa au anashindwa kuwasilisha taarifa, vitabu vya mahesabu, maelezo au nyaraka nyingine ambazo ziko mikononi mwake au katika mamlaka yake vimetajwa katika kuitwa kwake;
Atakuwa ametenda kosa na kama atapatikana na hatia atalipa faini isiyozidi shilingi elfu ishirini, au kifungo kwa muda usiozidi miezi sita au vyote kwa pamoja
Kifungu cha 33.1, mswada unasema, kama Mahakama itaamua kutoa tuzo ya fidia kwa hasara au gharama katika jambo lolote lile katika mamlaka yake, kama yule mnufaikaji atapeleka maombi ya kufanyiwa hivyo, itatoa hati ikieleza kiwango cha fidia au gharama
Na kifungu cha 33.2 kinasema kuwa kila cheti kitakachotolewa kwa mujibu wa kifungu (1) kitajazwa katika Mahakama Kuu na mnufaikaji, na baada ya kujazwa itahesabika kuwa ni amri ya mahakama kuu na itatekelezwa vilivyo
Isipokuwa kama itaelezwa vingine katika Sheria hii, kifungu cha 34, Jaji Mkuu kwa kushauriana na Mwenyekiti wa Mahakama, na kwa notisi katika gazeti la serikali, ataweka taratibu zinazolinda utendaji na uendeshaji wa Mahakama kwa kuzingatia malengo ya Makahakama
SEHEMU YA IX
VIFUNGU VINGINE
Likizo ya uzazi ya wanaume
Masuala ya utasa
Haki za mama za uzazi
Masuala ya uzazi na afya ya uzazi mahala pa kazi
Masuala ya afya ya uzazi kwa mama waliomo kifungoni
Masuala ya afya ya uzazi kwa mama wenye ulemavu wa akili
Emil Hagamu,
Mkurugenzi wa Pro-Life Tanzania,
February 28, 2012