Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika waraka wake, "Injili ya Uhai" anasema kuwa Injili ya Uhai ndiyo kiini cha mafundisho ya Yesu. Ni ujumbe ambao Kanisa huupokea siku hadi siku kwa moyo wa upendo, na ambao Kanisa halina budi kuuhubiri kiaminifu na kwa ujasiri kama "habari njema" kwa watu wa nyakati zote na tamaduni zote. Akiendelea, Baba Mtakatifu anasema kuwa Injili hii ya Uhai ambayo Kanisa imeipokea kutoka kwa Bwana wake ina nguvu na uwezo wa kupenya ndani kabisa ya moyo wa kila manadamu; mamoja kama ni mwumini au sivyo, kwani Injili hii ya Uhai siyo tu inakidhi kwa namna ya ajabu matarajio yote ya moyo bali pia inapita kabisa hata upeo wake. Kanisa linajiona kuwa limeitwa kuwahubiria watu wa nyakati zote "Injili" hii, ambayo ni chemchemi ya matumaini yasiyovunjika na furaha ya kweli kwa kila kizazi. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu, Injili kuhusu hadhi ya mwanadamu na Injili ya uhai ni wimbo mmoja usiogawanyika.