Ulimwengu umebadilika sana. Maendeleo makubwa yamefikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu. Katika sayansi binadamu ameweza kugundua mambo muhimu kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe na kwa ajili ya ustawi wa watu wa dunia.
Yeyote angedhani kuwa maendeleo haya katika teknolojiaa, yanaendana na maendeleo ya kweli ya binadamu mwenyewe, yaani pamoja nayo, makuzi thabiti ya kimaadili, kiutu, kiroho na kimwili. Kwa bahati mbaya sana, na kwa maangamizi ya binadamu mwenyewe, juhudi zinazofanywa katika nyanja za sayansi na teknolojia zina maelekeo ya kumwangamiza binadamu mwenyewe. Maendeleo hayo hasi yamefikia upeo wake na kuzaa kitu tunachokishuhudia sasa: utamaduni wa kifo.
Sera na mipango vimekua ambapo kwa njia ya ujanja; ulaghai na kifo vinaonyeshwa kama ni ukweli na uhai. Katika hali kama hii, tunahitaji tena kugundua upya thamani ya uhai wa binadamu na kupambanua kwa ufasaha ili kugundua tofauti kati ya utamaduni wa uhai na utamaduni wa kifo, jambo ambalo ndugu Emil Hagamu, katika kijitabu hiki amejaribu kulifanya kwa ufasaha kabisa.
Tunapomaliza kusoma kijitabu hiki, sote tunakuwa katika nafasi nzuri ya kuona namna gani kifo kinatukabili kupitia mfumo-mamboleo; na kujifunza namna ya kujali, kutetea na kulinda uhai wa binadamu.
Namwalika kila mtu mwenye mapenzi mema kusoma kijitabu hiki kwa lengo sio tu la kupata maarifa, bali zaidi sana kujengeka katika utamaduni wa uhai.
Joseph Ludovick
Dar es Salaam
SHUKURANI
Kazi hii ilikuwa kubwa na nzito. Ingechukua muda mrefu kama mtu mmoja peke yake angeitayarisha. Lakini, namshukuru Mungu, baada ya kushirikiana na wenzangu ofisini, kazi imechukua muda mfupi sana. Napenda kwa namna ya pekee niwashukuru wafuatao ambao walishiriki nami katika kuandaa kijitabu hiki: Bwana Joseph Ludovick ambaye amejiunga nasi baada ya kuacha Seminari Kuu ya Kibosho ambako alikuwa anasoma masomo ya falsafa; Bibi Grace Shayo Morrisson, ambaye ni Katibu Muhtasi hapa ofisini, na Bi Beatha Singano, ambaye ni mwandishi wa habari kitaaluma na ambaye anatusaidia hapa ofisini. Zaidi ya kukitayarisha pamoja, Bibi Grace Shayo Morrisson na Bi Beatha Singano ndio waliochapa katika komputa kazi hiyo na kuifanyia madoido kadiri walivyoona inapendeza.
Kama mtakavyokuwa mnasoma, nimetumia vitabu, vipeperushi na vijarida mbalimbali katika kukusanya habari na kuziweka katika mpangilio huu mnaouona. Napenda nichukue nafasi hii kumshukuru sana Sr. Dr. Birgitta Schnell, OSB, mkufunzi mwandamizi wa mpango wa uzazi kwa njia ya maumbile [asili] aliyeniruhusu ninukuu sehemu ya kitabu chake cha Uimarishaji wa Familia, Toleo la 2005 kwa ajili ya kuandaa mada ya Mpango wa Uzazi kwa kufuata Maumbile. Napenda pia niwashukuru waandishi wa vitabu na majarida ambayo nimetumia katika kukusanya taarifa na hivyo kuwawezesha wengine kupata maarifa na kufuata njia ya kweli. Natoa shukrani zangu kwa wasikilizaji wa Radio Maria [Sauti ya Kikristo Nyumbani mwako], ambao kwa njia ya vipindi vya Utetezi wa Uhai, waliniuliza maswali mengi kuhusiana na mada zilizoandikwa humu. Naamini watapata majibu baada ya kusoma kijitabu hiki.
Kijitabu hiki kinatolewa kwa lengo la kukidhi kiu ya watu waliopenda kupata habari sahihi na ya kweli juu ya vidhibiti mimba. Aidha kijitabu hiki kimejaribu kuandika masuala hayo kwa kina nikizingatia taarifa za kisayansi na nikizingatia pia mafundisho ya kimaadili na kiteolojia. Naamini kuwa wale wote watakaopata bahati ya kukisoma watanufaika na kupasisha ujumbe uliomo kwa wengine ambao hawakubahatika kusoma. Vilevile kijitabu hiki kitatumika kama kitini cha kufundishia mada za utetezi uhai na uimarishaji familia. Kwa kuweka wazi madhara ya vidhibiti mimba napenda kuwaalika wasomaji kutafakari kwa kina mpango wa Mungu katika uumbaji na nafasi ya mume na mke katika kujengana na kuidumisha ndoa yao.
Nawaalika nyote msafiri pamoja nami tukiyafunua maajabu ya Mungu katika uumbaji wa binadamu na katika kuyatiisha malimwengu. Ni wajibu wetu kuitika mwaliko wa Mungu wa kuwa watu wa uhai na kwa ajili ya uhai. Mimi na wewe tumepewa dhamana kubwa ya kutangaza na kudumisha Injili ya Uhai.